WEWE NI MTUMIAJI WA KOMPYUTA? FAHAMU KUHUSU SHERIA YA 20 20 20.

Ni wazi matumizi ya simu janja yameongezeka kwa kasi sana na kusababisha matumizi ya kompyuta kupungua kwa kiasi flani, lakini pia ni wazi kuwa kompyuta bado zinayo nafasi yake kubwa sana kwenye maisha ya kila siku hii ni kutokana na kuwa bado kuna mambo ambayo ni vigumu kuyafanya kwa kupitia kwenye simu zetu za mkononi. Ndio maana leo tumekuletea makala hii ya sheria ya 20 20 20 ambayo ni muhimu sana kwa afya yako kwa wewe mtumiaji wa kompyuta.

Wote tunajua matumizi ya kompyuta ya muda mrefu kuna wakati haya epukiki, iwe umeajiriwa au wewe ni mwanafunzi ni lazima utatumia kompyuta kwa muda mrefu kwa namna moja ama nyingine. Sasa matumizi haya ya muda mrefu husababisha matatizo mbalimbali kwenye mwili wetu kuanzia kwenye macho hadi sehemu nyingine za mwili kutokana na kukaa sana.

Baadhi ya matatizo au dalili zinazo patikana kwa kutumia kompyuta kwa muda mrefu ni pamoja na macho kuwa kama yanawaka moto au kuwasha, kichwa kuuma, kutokuona vizuri au kuona ukungu pamoja na matatizo mengine ya muda mfupi ambayo kwa ujumla wake  yamepewa jina la kitaalam la Computer Vision Syndrome, Kwa mujibu wa mtandao wa WebMD bado hakuna ushahidi kwamba utumiaji wa kompyuta kwa muda mrefu unaweza kusababisha upofu badala yake watafiti hao wamegundua kuwa unaweza kusababisha matatizo mbalimbali ambayo ndio kwa ujumla wake yanaitwa Computer Vision Syndrome.

Lakini pamoja na hayo kuna njia za kujilinda usipate matatizo hayo, njia moja muhimu na inayo shauriwa na wataalamu wengi ni pamoja na sheria ya 20 20 20. Hii sio sheria mpya bali ni sheria inayotumiwa na watu wengi sana kwa sasa japo kwa hapa kwetu sidhani kama inatumika kwa upana wake kama inavyotakiwa. Sasa ili uweze kuelewa nitatumia mchoro hapo chini kuweza kukuelewesha na natumaini utaweza kufuata sheria hiyo rahisi itakayo saidia macho yako kuwa salama pamoja na kujilinda na Computer Vision Syndrome.

Sasa basi maana ya Sheria ya 20 20 20 ni kuwa, endapo una angalia kompyuta kwa muda mrefu, unatakiwa kupumzisha macho yako kila baada ya dakika 20 (ishirini) na wakati huo unatakiwa kuangalia kitu kilichopo umbali wa futi 20 (ishirini) kutoka mahali ulipo na unatakiwa kuangalia kitu hicho kwa sekunde 20 (ishirini). Hiyo ndio maana ya 20 20 20.

Sasa najua utaniuliza kwanini sekunde 20..? Kwa mujibu wa tovuti ya Healthline, macho hutumua sekunde 20 kuweza kupumzika kikamilifu hivyo ni muhimu sana kuhakikisha unafuata sheria hii. Watalamu mbalimbali wa maswala ya macho duniani wana shauri sana sheria hii na ni muhimu sana kuhakikisha unaifuta pamoja na kupumzisha mara kwa mara macho yako hasa kwa wale wafanyakazi wa maofisini ambao huangalia karatasi nyeupe na baadae kuangalia kioo cha kompyuta.

Mpaka hapo natumaini utakuwa umefahamu sheria ya 20 20 20, hakikisha unatumia sheria hii maana ni kweli inasaidia sana na pia hakikisha unapata muda wa kupumzika au kumpizisha macho yako hii itakusaidia kiafya na pia kiutendaji.

0 Comments

Je unamaoni kuhusu makala uliyoisoma dondosha maoni yako hapa