Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, janga la Covid "litaendelea kwa mwaka mmoja zaidi " kwa sababu nchi masikini hazipati chanjo zinazohitajika kwa ajili ya kukabiliana na virusi vya Corona.
Dkt. Bruce Aylward, kiongozi mwandamizi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) amesema kuwa, kutokana na mwenendo huu wa kutopata nchi masikini chanjo ya kukabiliana na virusi vya Corona inamaanisha janga la Covid linaweza "kujivuta kwa urahisi hadi 2022".
Chini ya 5% ya idadi ya watu wa Afrika wamepewa chanjo, ikilinganishwa na 40% katika mabara mengine ulimwenguni .
Mataifa mbalimbali ya Kiafrika yamekuwa yakilalamikia dhulma na ukosefu wa uadilifu unaoshuhudiwa katika suala la ugavi wa chanjo za corona na yamekuwa yakitoa wito wa kutolewa msaada wa kivitendo ili kutimiza lengo la Shirika la Afya Duniani (WHO) la kutoa chanjo kwa asilimia 40 kwa watu wote duniani hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa 2021.
Aidha asasi za kimataifa kama Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa nazo zinalalamikia ugavi usio wa kiadilifu wa chanjo za ugonjwa wa Covid-19 duniani na kusisitiza kuwa zinatiwa wasiwasi na uhaba wa chanjo hizo katika baadhi ya nchi maskini duniani.
Karibu watu milioni 5 wameaga dunia ulimwenguni kote kufuatia janga la Covid-19 huku walioambukizwa hadi sasa wakikaribia milioni 250. Marekani ndio nchi iliyoathiria zaidi na janga la Corona ambapo watu zaidi ya laki 7 na nusu wameaga dunia huku walioambukizwa wakipindukia milioni 46. India, Brazil, Uingereza na Russia zinafuatia katika orodha hiyo. Barani Afrika nchi ya Afrika Kusini ndio iliyoathiriwa zaidi na janga la Corona ikifuatiwa na Morocco na Tunisia.
0 Comments
Je unamaoni kuhusu makala uliyoisoma dondosha maoni yako hapa