KAMPUNI YA UBER YAJA HUDUMA YA UBERBOAT DAR NA ZANZIBAR

Kampuni ya Uber ambayo inaongoza kwa kutoa huduma za usafirishaji wa abiria kwa njia ya kisasa, hivi karibuni imetangaza kuwa inajiandaa kuja na huduma mpya ya Uberboat ambayo kwa hatua ya awali itawasaidia wakazi wa jiji la Dar es salaam pamoja na Zanzibar.

Akiongea kwenye tamasha la uzinduzi wa huduma hiyo jana uliohusisha watu mbalimbali ikiwa madereva wa Uber pamoja na balozi wa brand ya Uber Tanzania ( Brand Ambassador ), Idris Sultan, Meneja masoko wa Uber Afrika Mashariki, Ms Elizabeth Njeri alisema uamuzi wa kuleta huduma hiyo mpya ya Uberboat umekuja baada ya kuona huduma za Uber Taxi na Uber Poa zinafanya vizuri kadri siku zinavyokwenda.

Hata hivyo Meneja huyo hakutangaza tarehe halisi ya ujio wa huduma hiyo mpya ya Uberboat ila alisema kuwa huduma hiyo inategemewa kuja siku za karibuni hapa Tanzania. “Dar es Salaam imezungukwa na fukwe nzuri lakini wakazi hawawezi kufurahia fukwe hizo kwa sababu hawajui jinsi ya kufika huko. Uberboat ambayo itazinduliwa hivi karibuni itaziba pengo hilo,” alisema bila kutaja tarehe ya uzinduzi halisi.

Bado mpaka sasa haijajulikana jinsi huduma hiyo itakavyo kuwa inafanyakazi lakini inasemekana huduma hiyo haitakuwa tofauti sana na utaratibu ulioko sasa unaotumika kwenye Uber Tax na Uber Poa. Kwa habari zaidi kuhusu Uberboat endelea kutembelea SwahiliTech.net tutakujuza zaidi.

0 Comments

Je unamaoni kuhusu makala uliyoisoma dondosha maoni yako hapa