FAHAMU SIMU MPYA YA KUKUNJA YENYE VIOO VIWILI SAMSUNG GALAXY W2018

As salaam aleikum. Je, unakumbuka simu za mkunjo za kipindi cha miaka ya 90 na 2000? Kama ndio basi zimerudi tena lakini katika kiwango cha ubora wa juu, muonekano wa kuvutia zaidi pamoja na teknolojia ya kisasa.

Kampuni ya Samsung ikishirikiana na China Telecom imetangaza uzinduzi wa simu ya bei ghali ya mkunjo yenye vioo viwili inayofahamika kama Samsung W2018.

Uzinduzi wa simu janja hiyo umefanyika Desemba mosi mwaka jana huko Xiamen, nchini China ukiambatana na sherehe za kutimia miaka 15 ya toleo la familia ya W kwa simu za Samsung Galaxy na miaka 25 ya soko la Samsung nchini China.

Samsung W2018 ambayo sifa zake za ndani inafanana sana na Sansung Galaxy S8, inakuja na kioo cha ukubwa wa nchi 4.2 chenye teknolojia ya AMOLED pamoja na RAM yenye ukubwa 6GB na ukubwa wa uhifadhi wa ndani wenye ukubwa wa 64GB na 256GB.
Uzuri wa simu hii utaweza kutumia aidha kioo cha nje au ndani baada ya kuikunjua simu yako. Mfano unaweza kutumia kioo cha ndani na ukabadili kwa kutumia kioo cha nje kwa kazi ileile iliyokuwa kwenye kioo cha ndani na ukaendelea nayo ama ukaendelea na kitu kingine kipya.

Pia itakupa na uwanja mpana wa kutumia baobonye/kicharazio (keyboard) halisi au ya kugusa (Touch).

Ukubwa wa Betri katika Samsung W2018 ni 2,300mAh na itakuwa na mfumo endeshi wa Android Nougat. Simu hiyo itakuwa katika rangi nyeusi, Fedha na Dhahabu.

Kwa upande wa kamera kutakuwa na kamera ya nyuma yenye 12MP na kamera ya mbele yenye 5MP na kuweza kurekodi video kwa teknolojia ya 4K. Simu hiyo itaendeshwa na  prosesa ya Snapdragon 835.

Hata hivyo kikwazo kikubwa cha simu hiyo ni bei yake. Kama ulidhani iPhone X ni ghali zaidi, basi kwa Samsung W2018 ni ghali zaidi.

Ingawa bei haijawekwa rasmi lakini inaelezwa bei ya Samsung W2018 itauzwa kwa Dola za kimarekani 2,400 ambazo ni takribani Tsh 5,399,040 ambazo pesa hizo zinamuwezesha Mtanzania wa kawaida kumudu kununua kiwanja cha ukubwa mzuri kilichopimwa na serikali.

Hii sio simu janja ya kwanza ya Samsung Galaxy kuwa ya mkunjo. Simu janja ya mkunjo nyingine ilizinduliwa mapema mwaka huu inayofahamika kwa jina la Samsung leadership 8 ambayo nayo inapatikana kwa soko la China pekee.

Simu ya Samsung W2018 kwa sasa itapatikana katika soko la China pekee na hakuna taarifa rasmi kama itapatikana katika masoko mbalimbali katika nchi zingine.

Nini maoni yako kuhusiana na makala haya. Je una swali lolote. kwa maoni au maswali kuhusu makala haya usisite kutuandikia hapo chini nasi tutakujibu haraka iwezekanavyo.

0 Comments

Je unamaoni kuhusu makala uliyoisoma dondosha maoni yako hapa