KWANINI iPHONE ZINAKITUNDU CHEUSI NYUMA KATI YA KAMERA NA FLASH?

As salaam aleikum, Inawezekana ukawa mmoja wa watumiaji wa iPhone kwa kipindi sasa na unafahamu mambo mengi sana kuhusiana na simu hizi kutoka kampuni ya Apple. Swali je, ushawahi kuona kitundu cheusi katikati ya kamera ya flash, unafahamu matumizi yake?

Kwa kifupi kuanzia toleo la iPhone 5 kila simu ya iPhone baada ya toleo hili ina kitundu cheusi katikati ya kamera na flash. Kimsingi kitundu hicho ni Microphone. Ndio ni Microphone inayotumika kupunguza mwingiliano wa mawimbi ya sauti.

Microphone (kinasa sauti) hii imewekwa maalumu kwa ajili ya kupunguza mwingiliano wa mawimbi ya sauti ili kumwezesha msikilizaji wa upande wa pili wa simu asisikie vitu vingine tofauti na kile kinachozungumzwa na mwongeaji mwenza.

Haijawahi kukutokea unaongea na mtu kwenye simu alafu kwa mbali unasikia sauti za watu wengine walio karibu yake? Au kukatishwa maongezi na mtu uliyempigia kwa sababu yupo kwenye daladala au sehemu yenye purukashani nyingi? Sasa hapo ndipo hiyo Microphone inapofanya kazi yake, itanasa mawimbi yote ya sauti yasiyohusika na kupunguza mwingiliano wakati mtumiaji wake anaongea na simu.

Kwa kifupi iPhone zote kuanzia iPhone 5 zina vinasa sauti vitatu (3 Microphones), viwili vikiwa chini ya simu na kimoja kikiwa nyuma ya simu. Uwepo wa programu ya Siri inayohitaji kinasa sauti kizuri ili kuweza kutambua mzungumzaji ameongea nini kunachangia sana kuwekwa kwa microphone hizi tatu.

Nadhani sasa utakuwa umeelewa kwanini iPhone ina kitundu cheusi katikati ya Kamera na Flash.

0 Comments

Je unamaoni kuhusu makala uliyoisoma dondosha maoni yako hapa