Fahamu njia hizi tatu za kujipatia pesa youtube bila kujiunga na adsense

As salaam aleikum mpendwa mfuatiliaji wa tovuti yetu hii pendwa ya Riyadi Bhai leo tuangalie njia tatu tofauti za kutengeneza pesa kupitia youtube bila ya adsense Watengenezaji wengi wa video wanajua jisi ilivyo vigumu kutengeneza pato la uhakika kupitia Youtube kwa kutumia Adsense pekee. Watengenezaji wengi wa video wamekuwa wakifikiri kuwa kupakia video zenye ubora sana kwenye mtandao wa YouTube kutawafanya kupata fedha lakini mambo yamekuwa tofauti mno na matarajio.



Ni vigumu kujua ni kiasi gani unaweza kupata kutokana na Adsense kwenye YouTube, lakini unaweza kukadiria kwa video kutazamwa mara elfu moja utapata takribani dola moja. Kiasi hiki ni kidogo ukilinganisha na kazi utakayokuwa umeifanya ili kukipata.


Tazama njia tatu nitakazokueleza zitakazokuwezesha kupata fedha kwenye mtandao wa YouTube bila kutumia Adsense.


1. Mshirika au Wakala

Unaweza kupata fedha kwenye YouTube kwa njia ya kuwa mshirika au wakala wa makapuni mbalimbali yanayozalisha au kuuza bidhaa.


Hili linafanyika kwa kuweka kiunganishi (link) ndani ya video au chini ya video kinacholenga bidhaa fulani. Endapo mtu atanunua bidhaa hiyo kupitia kiunganishi (link) yako, basi utapata gawio/faida yako kutokana na kuuzwa kwa bidhaa husika.


Unaweza kujiunga na huduma hii kwa kutumia mitandao inayokubali ushirika/uwakala kama vile Amazon , eBay, n.k.


2. Uza Bidhaa Zako Mwenyewe

Wengi tunafahamu kuwa YouTube huwatoza wauzaji wa bidhaa na huduma kisha kuwalipa wale ambao video zao zimetumika kutangaza bidhaa au huduma hizo. Mchakato huu ni mrefu wenye kuhusisha watu wengi, hivyo si rahisi kupata fedha za uhakika.


Lakini kama unazalisha bidhaa zako ni vyema ukatumia Chaneli yako kuzitangaza kwani kwa njia hii hutotozwa gharama za matangazo. Hivyo basi utaweza kupata wateja na kujipatia fedha zaidi.


Laini pia, video yako ikiwa na watazamaji 800 au 900 na 10 kati yao wakanunua bidhaa yako ya Sh. 10,000 utakuwa umepata Sh. 100,000 tayari; lakini kwa Adsense ungepata dola 1 tu kutokana na watazamaji 1,000.


3. Ushauri na Ukufunzi

Je una maarifa ya kuwashauri watu katika jambo fulani au unaweza kufundisha jambo fulani? Kama jibu ni ndiyo, basi fursa iko mkononi mwako. Unachotakiwa kufanya hapa ni kuandaa video nzuri za kushauri watazamaji wako au kuwafundisha mada fulani.


Utakapokuwa umeaminika na umepata watazamaji wengi, ni rahisi kuwaambia wajiunge na huduma yako ili kupata mafunzo zaidi. Unaweza kuwatoza fedha kiasi fulani ili kupata mada nyingi au kubwa zaidi.


Kama utakuwa unafanya vizuri ni rahisi sana watazamaji kulipia huduma hiyo kwani wanajua unavyofanya vyema kwenye video ulizotoa bure; hivyo wataamini video za kulipia zitakuwa bora zaidi.

0 Comments

Je unamaoni kuhusu makala uliyoisoma dondosha maoni yako hapa