WHO yasisitiza udharura wa kupewa chanjo wahudumu wa afya

Shirika la Afya Duniani WHO limesisitiza udharura wa kupewa kipaumbele wahudumu wa afya katika utolewaji chanjo ya corona na kusema, ukweli kwamba mamilioni ya wahudumu wa sekta ya afya bado hawajapokea chanjo hiyo ni onyo la uhalifu dhidi ya nchi na mashirika yanayodhibiti usambazaji wa chanjo hiyo.

Akizungumzia suala hilo hapo jana usiku akiwa mjini Paris Ufaransa, Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkuregenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO, amekosoa kutokuwepo usawa katika usambazaji wa chanjo ya corona ulimwenguni na kusisitiza kwamba tuimu za wahudumu wa afya zinapasa kupewa kipaumbele katika utolewaji wa chanjo hiyo.


Adhanom amesema kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na nchi 119 kwa wastani kati ya wahudumu wa afya watano, ni wawili tu kati yao ndio waliopewa dozi kamili ya kukabiliana na maradhi ya corona.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO amesema barani Afrika ni chini ya mhudumu mmoja kati ya kumi ndiye amepewa dozi kamili ya kukabiliana na corona katika hali ambayo katika nchi nyingi tajiri, zaidi ya asilimia 80 ya wahudumu wa afya tayari wamekwishapata dozi kamili ya kupambana na virusi hivyo.

Kwa mujibu wa tovuti ya WorldoMeter ambayo hutoa takwimu za karibuni zaidi kuhusiana na watu walioambukizwa virusi vya corona, kufikia Ijumaa zaidi ya watu milioni 243 na laki 40 walikuwa wameambukizwa virusi vya corona duniani na zaidi ya milioni 4 na laki 9 kupoteza maisha kutokana na maradhi hayo.

Kwa mujibu wa takwimu hizo Marekani, India, Brazil, Uingereza, Russia na Uturuki ndizo zinaongoza duniani kwa wingi wa watu waliombakizwa virusi hivyo.

0 Comments

Je unamaoni kuhusu makala uliyoisoma dondosha maoni yako hapa