Li-Fi Technology; Mbadala wa Wi-Fi Katika Intaneti, Ikiwa na Kasi Mara 100 Zaidi ya Wi-fi

As salaam aleikum Yawezekana umewahi kusikia kuhusu teknolojia ya Wi-Fi na pengine na wewe ni miongoni mwa wanaotumia teknolojia hii. Kama hujui, hii ni teknolojia inayokuwezesha kupata intaneti kwenye simu yako ya mkononi, tablet, kompyuta au vifaa vingine vyote vinavyotumia intaneti.

Kwa kutumia Wi-Fi, unaweza kutazama video mtandaoni, unaweza kusikiliza muziki, kuingia kwenye mitandao ya kijamii, Instagram, Facebook, WhatsApp, Snapchat na mitandao mingine kibao. Kwa kifupi, unaweza kufanya kila kitu kinachohusianana intaneti bila kuwasha ‘data’ kwenye simu yako.

Unachotakiwa ni kuwa tu sehemu yenye Wi-Fi, kisha unaji-connect kwa kupitia simu yako au kifaa chochote kinachotumia intaneti na unaendelea kuperuzi kwenye mitandao kwa kasi kubwa pengine kuliko ukitumia ‘data’, kutegemea na uimara wa Wi-Fi mahali ulipo.

Wakati Wabongo wengi ndiyo kwanza wameanza kuishtukia teknolojia hii na kuanza kuitumia kwa kasi, kwenye maofisi mengi kukiwa kumefungwa vifaa maalum vya kukuwezesha kupata Wi-Fi bila chenga, nchi za wenzetu tayari kilishakuwa kitu cha kawaida sana na yapo baadhi ya majiji ambayo unapata Wi-Fi ya bure popote ulipo!

Kwa jinsi dunia inavyokwenda kasi, wakati sisi ‘tukihangaika’ na Wi-Fi, tayari wanasayansi kwenye nchi zilizoendelea, wamegundua teknolojia mpya, yenye kasi ya zaidi ya mara mia moja ya Wi-Fi ya kawaida.

Teknolojia hii inaitwa Li-Fi (Light Fidelity) na tofauti na Wi-Fi inayotumia mawimbi ya radio (radio waves), Li-Fi inatumia mawimbi ya mwanga (Light Waves).

Kinachofanyika ni kwamba, taa maalum (LED Light) ndizo zinazotumika kusambaza mawimbi ya Li-Fi na watu waliopo ndani ya eneo ambalo mwanga wa taa hiyo unafika, wanakuwa na uwezo wa kupata intaneti yenye kasi kama ya mwanga! Yaani hata kama video ni kubwa kiasi gani, ukitaka kudownload, unagusa tu na ndani ya sekunde chache kazi inakuwa imeshakwisha.

Taa hizo huwa zinaunganishwa na kifaa maalum ambacho ndicho kinachopokea intaneti kutoka kwenye satelite, kisha kinaibadilisha kwenda kwenye mawimbi ya mwanga na kuisambaza kupitia taa hizo, ambazo zinatakiwa kuwashwa muda wote ili kupata intaneti. 
Kasi ya Li-Fi, ni 224 gigabits/seconds na kama nilivyokueleza, ni zaidi ya mara 100 ya Wi-Fi ya kawaida. Mgunduzi wa teknolojia hii ni Profesa Harald Haas wa Chuo Kikuu cha Edinburgh nchini Uingereza na tayari imeshafanyiwa majaribio nchini Uingereza, Marekani, Dubai na maeneo mengine duniani.

Changamoto kubwa ni kwamba, ili kuwahudumia watu wengi zaidi, taa zinatakiwa kuwa nyingi na zinatakiwa kuwashwa muda wote, hata mchana. Pia Li-Fi haina uwezo wa kuvuka ukuta, taa ikiwashwa ni wale tu waliopo ndani ya eneo mwanga unapofika ndiyo watakaopata intaneti.

Ili kukabiliana na tishio la Li-Fi inayoonekana kama itakuja kuliua soko la Wi-Fi, Kampuni inayotoa huduma za Wi-Fi ipo mbioni kuanza kutumia teknolojia mpya iitwayo Wi-Fi HaLow ambayo nayo itakuwa na kasi kubwa zaidi ambayo hata hivyo, bado haitaifikia Li-Fi.

Tayari makampuni makubwa kama PureLiFi, Lucibel, Icade na Phillips pamoja na Jeshi la Marekani yameongeza nguvu na kuanza katika project hiyo kubwa na kuanza kutengeneza vifaa vyenye uwezo wa kupokea mawimbi ya Li-Fi na matarajio ni kwamba mpaka ikifika 2020, Li-Fi itakuwa imesambaa dunia nzima.

0 Comments

Je unamaoni kuhusu makala uliyoisoma dondosha maoni yako hapa